Sunday, December 13, 2015

Soma

Kijana mmoja alitokea kumpenda sana dada mmoja ijapokuwa dada huyo alikuwa akimtolea nje mara kwa mara lakini kijana hakukata tamaa, akiendelea kurusha ndoano huku akiamini siku moja atafanikiwa.Siku moja dada huyo akiwa yupo nyumbani aliamua kumpigia simu huyu kaka na kumtaka aje nyumbani kwake, yule kijana alifurahi na kuhisi sasa ombi lake limekubaliwa.
Akiwa nyumbani kwake dada huyo , alikuwa amevalia kanga moja laini, kutokana na hali ya hewa ya joto la Dar es salaam.Kwa upande wa yule kijana alikuwa amefurahi sana na haraka alijiandaa na kuanza safari kuelekea kwa huyu dada, njia ni kaka huyu alikuwa akijiuliza maswali mengi, huku akiwa haamini kama yule dada amemuita nyumbani kwake. Alipofika, alibisha hodi na yuel dad a akafungua mlango huku akionyesha tabasamu pana katika paji la uso wake.
Kaka huyu aliingia ndani huku kijasho kikimteremka mithili ya mtu aliyekuwa anakimbia. Dada huyu alimkaribisha vizuri, yule kaka aliomba maji ya kunywa huku muda wote akimtizama kwa umakini dada huyu mrembo, aliyeumbika kila idara na ile kanga nyepesi aliyovaa ilikuwa ikionyesha umbo zuri la dada huyu ambaye waswahili huwa wanasema, mtoto kajaaliwa (mashalaah) Kaka alikuwa akivuta pumzi kwa haraka haraka, na kusema "Nimefurahi sana, umenikaribisha nyumbani kwako ni pazuri sana." Yule dada alitabasamu na kusema "Asante sana, nimefurahi pia umeitikia wito wangu, samahani kwa usumbufu wangu".
Yule kaka alitabasamu huku akijisogeza sogeza "Hakuna tatizo, usijali kabisa, mimi nipo kwa ajili yako, naimani sasa nina...." Kabla hajamilizia kuongea yule dada alimshika mikono yake miwili huku akimtizama machoni, kwa macho yake malegevu, mithili ya mtu aliyekula kungu "Samahani kaka, mimi nimekuita hapa kuna jambo nataka unishauri, nataka kujua ni zawadi gani nzuri unaweza kumpatia mwanaume unayempenda" Kaka yule alikuwa akitetemeka na kusema "Chochote tu, zawadi ni zawadi, alimradi kuwe na mapenzi ya kweli" Dada yule alitabasamu na kusema "Ni kweli, mapenzi ya kweli ndiyo jambo la msingi, nitampenda maisha yangu yote" Kaka yule akauliza "Utampenda? Nani huyo"
.
Yule dada alitabasamu tena na kusema "Samahani, rafiki nilikuwa sijakuambia, wiki ijayo nafunga ndoa na mpenzi wangu wa muda mrefu ambaye nampenda sana, na pia nilikuita ili nikupe kadi ya harusi, nitafurahi kukuona, kwani wewe ni rafiki yangu pia" Yule kaka alibaki amepigwa na butwaa, "Ati, nini unaolewa, daaah, jamani, kwahiyo." Alinyanyuka na kuondoka bila ya kuaga huku akimuacha yule dada anamuita ili ampatie kadi bila ya mafanikio.
SIYO KILA UNACHOKIWAZA MOYONI MWAKO KITATOKEA KAMA UNAVYOTAKA. KWAHIYO NI VYEMA KUJIANDAA KUKUBALIWA AU KUKATALIWA
FACEBOOK
“"Reshmail Manyama want to be your friend.'confirm' 'ignore' ulikuwa ni ujumbe ambao macho yangu yalikutana nao nilipofungua mtandao wa kijamii wa ‘facebook’,sikumbuki kama nilijifikiria mara mbili kwani niliona ni jambo la kawaida sana kukutana na 'notifications’ kama hizo,na mara zote neno confirm(kubali) lilipata fursa ya kutumika.hivyohivyo hata kwa Reshmail nilifanya hivyo."You and reshmail are now friends" ndio ujumbe ulionisindikiza baada ya kukubali ombi lile kutoka kwa Reshmail.
* * * * *
Ni kijana mtanashati niliyebahatika kukutana nae pale chuo kikuu cha mtakatifu Augustine Mwanza,alijipenda kuanzia ndani ya chumba chake hadi mwili wake,ilikuwa ni nadra sana kumfumania akiwa amevaa nguo aliyoivaa jana,bila kumnyima haki yake nasema alikuwa anapendeza kila siku,macho yangu ya kipelelezi na kamera zangu za kipaparazi kamwe hazikufanikiwa kumjua aliyekuwa ubavu wa pili wa bwana huyu yaani 'MPENZI'. Ukipenda waweza kuniita kimbelembele lakini ukiniita hivyo basi majina hayo yatakuwa mengi pale chuoni kwani wengi walikuwa na shauku kubwa ya kujua siri hiyo na kamwe hawakufanikiwa.
Binadamu hatuna dogo watu washaanza kusema eti huenda jamaa ana matatizo makubwa tu mwilini mwake ndio maana yuko peke yake licha ya kushobokewa na wasichana warembo, mh! mimi sikuwa mmoja wao lakin nilijiuliza pia kulikoni??
Makala mbovu zilizokuwa zinaandikwa na gazeti la chuo lililojulikana kama ‘Saut voice’ ndo zilinizonivuta zaidi kutaka na mimi siku moja kuandika katika gazeti hilo lililokosa mvuto siku za hivi karibuni makala nzuri itakayorudisha heshima ya gazeti hilo.Taratibu nilijenga mazoea na hatimaye nikafanikiwa kumzoea "THE MOST WANTED" ucheshi wangu ndio uliomvutia zaidi kupenda kuwa karibu nami pamoja na mchezo wa mpira wa miguu kwani wote tulikuwa mashabiki wakubwa,haukupita mwezi mzima nikawa nina uwezo wa kuanza kazi yangu,ni mimi na Adam Michael kwenye meza moja chumban kwangu ananipa hadithi yake ya maisha yaliyomfanya awe kama alivyo.
"Aah!! jamani Reshmail..." alianza Adam,yangu masikio na macho nikaanza kusikiliza kwa makini.
** ** **
Hadithi ya Joka Jeupe
K atika enzi za kale, kwenye Mlima wa Emi kulikuwa na majoka mawili yenye umri wa miaka elfu moja, moja jeupe, moja jeusi. Majoka hayo mawili yalipenda sana mandhari ya watu wanapoishi, basi yalijibadilisha kuwa wasichana wawili warembo, moja lilijipa jina la Bai Suzhen
, jingine liliitwa Xiao Qing. Siku moja walifika kwenye sehemu maarufu yenye mandhari nzuri, ziwa la Xihu mjini Hangzhou.
Mandhari ya ziwa la Xihu kweli ilivutia sana, walipofika kwenye daraja moja la ziwa hilo ghafla mvua ilianza kunyesha, wakakimbia mvua na kujificha chini ya mti mmoja mkubwa. Wakati huo alikuja kijana mmoja mwenye mwamvuli aliyeitwa Xuxian, ambaye alikuwa akirudi nyumbani baada ya kusafisha makaburi. Alipoona wasichana chini ya mti aliwasaidia kwa mwamvuli wake na baadaye aliwasaidia kuwapeleka nyumbani kwa mashua. Bai Suzhen alianza kumpenda kijana huyo, alipoagana na kijana huyo alimwambia kesho aje kuchukua mwamvuli wake.
Siku ya pili kijana Xuxian alifika nyumbani kwa Bai Suzhen karibu na ziwa kuchukua mwamvuli wake. Bai Suzhen alimshukuru sana na kumwuliza habari za familia yake, akafahamu kuwa alifiwa na wazazi wake mapema tokea alipokuwa mtoto na sasa anaishi kwa dada yake na kufanya kazi katika duka moja la dawa. Msichana Bai Suzhen aliomwomba aolewe naye. Hakika Xu Xian alikuwa na furaha isiyo kifani. Kwa kuongozwa na Xiao Qing walifanya sherehe ya ndoa. Baada ya ndoa walianzisha duka la dawa. Bai Suzhen alifahamu matibabu, kila siku aliwatibu wagonjwa wengi.
  Kulikuwa na sufii mmoja wa dini ya Buddha aliyekuwa anaitwa Fa Hai. Fa Hai alikuwa anajua siri ya Bai Suzhen kuwa alikuwa joka mwenye miaka elfu moja, na hakika angewadhuru watu, hivyo alidhamiria kumwokoa kijana Xu Xian.
Siku moja Fa Hai alikuja nyumbani kwa Xu Xian, alimwambia, mkewe ni zimwi. Xu Xian hakuamini. Basi Fa Hai alimwambia, kama haamini, ajaribu kumshawishi anywe pombe tarehe 5 Mei, siku ya mashindano ya mbio za mashua, na kama akinywa atarudia asili yake.
Tarehe 5 Mei ilifika, kila familia hunywa pombe kusherehekea siku hiyo. Majoka yanaogopa pombe, Bai Suzhen alitaka kwenda mlimani kukwepa, lakini alikuwa na wasiwasi kuwa mumewe Xu Xian atamshuku, alikuwa hana budi ila kubaki nyumbani akijidai anaumwa.
Ingawa Xu Xian hakuamini aliyoambiwa na sufii Fa Hai, lakini kila mmoja katika siku hiyo hunywa pombe, hivyo alimshawishi mkewe anywe pia. Mkewe Bai Suzhen alishindwa kukataa, alikunywa glasi moja, mara akaanza kuona kizunguzungu. Xu Xian alimsaidia hadi kitandani, kisha akaenda jikoni kumtengenezea supu ya kuondoa ulevi. Akaja na bakuli moja la supu kitandani, alipofungua chandarua akaona joka kubwa jeupe limelala kitandani, Xu Xian alikufa kwa mshtuko.
Joka jeupe lilipozinduka likaona mumewe amekufa kwa mshtuko, alihuzunika sana, alimwomba Xiao Qing amtunze mumewe, na yeye akatoka haraka na kwenda kwenye mlima mmoja ulioitwa Xianshan ambako kulikuwa na aina moja ya jani la dawa ambalo lingeweza kumwokoa mumewe.
Wakati huo Bai Suzhen alikuwa amepata mimba ya miezi saba. Alipofika mlima Xianshan watoto waliokuwa wananlinda mlima walipojua kuwa anataka kuiba jani la ajabu walipambana naye. Mungu wa mlima huo alipoona jinsi Bai Suzhen alivyohangaika kumwokoa mumewe alimpa jani la ajabu.
Xu Xian alifufuka, lakini bado alikuwa ameshikwa na hofu. Bai Suzhen alipatia mzungu wa kumdanganya, alitumia kitambaa kirefu cheupe na kukigeuza kuwa joka kuzunguka kwenye boriti la dari na kumwita mumewe aone. Kwa kuona joka hilo, Xu Xian aliondoa mashaka yake juu ya mkewe, na waliendelea kuishi kwa mapenzi.
Sufii Fa Hai hakukufa moyo. Siku moja alimdanganya Xu Xian kwenda kwenye hekalu lake na kumzuia asirudi nyumbani. Baadaye mkewe na Xiao Qing walikuwa kwenye hekalu wakitaka kumrudisha nyumbani, wakagombana na sufii. Wakati walipopurukushana, Bai Suzhen alisikia maumivu ya uja uzito, kwa haraka alirudi nyumbani na Xiao Qing, alipofika kwenye daraja alikumbuka jinsi alipokutana na mumewe na kuanza na mapenzi, alihuzunika sana. Xiao Qing alimlaumu Xu Xian kwa kumsikiliza sufii, alimshawishi Bai Suzhen amwache mumewe.
Kwa kusaidiwa na sufii wengine, Xu Xian alitoroka kutoka hekalu na kwenye daraja alimpata mkewe. Mkewe alimwambia ukweli wa mambo, kwamba kweli alikuwa joka. Wakati huo Xu Xian alikuwa ameelewa kwamba mapenzi ya mkewe ni ya kweli na makubwa, akamwahidi kuwa hatajali akiwa ni kitu gani, lakini ataishi naye mpaka kufa.
Baada ya kurudi nyumbani, muda mchache baadaye Bai Suzhen alizaa mtoto. Katika siku ya kutimiza mwezi mzima kwa mtoto walifurahi sana, lakini wakati huo sufii Fa Hai alikuja tena nyumbani, alimkamata Bai Suzhen na kumtia chini ya mnara wa Leifong kando ya ziwa la Xihu.
Xiao Qing alitorokea mlimani Emei, alijitahidi kuinua uhodari wake wa mapambano, mwishowe alimshinda Fa Hai, na alimwokoa Bai Suzhen.
SIMULIZI YA KWELI YA KUSISIMUA NA KUSIKITISHA YA MTOTO JANETH :
Kengele ya kutoka darasani iligongwa, wanafunzi wa shule ya msingi wakaanza kutoka madarasani huku wakifukuzana wengine wakipiga kelele ilimradi shwangwe tu.
Ilikuwa mara yangu ya kwanza kufundisha shule za hatua hiyo.
Ilikuwa ni shule ya serikali.
Jicho langu liliangukia katika sura ya msichana mdogo, nguo zake chafu. Alikuwa analia.
Alikuwa peke yake na hakuwa na yeyote wa kumbembeleza.
Mimi kama mwalimu sikutaka kujisogeza karibu naye sana. Kwanza nilikuwa mgeni.
Nikaachana naye.
Siku iliyofuata tukio kama lile likajirudia. Msichana yuleyule wakati ule uleule wa kutawanyika, alikuwa analia sana. Mwishowe aliondoka huku akiwa analia.
“Mbona mwenzenu analia?” nilimuuliza mwanafunzi mmoja.
“Huyo ni mama kulialia..” alinijibu huku anacheka.
Haikuniingia akilini hata kidogo kuwa yule binti analia bila sababu.
Siku ya tatu nikaanza kujiweka karibu naye.
Muda wa mapumziko nilimwita nikamnunulia chai, alikuwa ananiogopa na hakutaka kuniangalia machoni.
Sikumuuliza lolote juu ya tabia yake ya kulia lia kila anaporuhusiwa kurejea nyumbani.
Hata siku hiyo pia alilia vilevile. Wenzake wakawa wanamzomea.
Akili yangu iligoma kuamini kuwa binti yule analia bila sababu.
Kwanini alie wakati wa kutawanyika tu?? Hapana si bure.
Nikaendelea kujiweka karibu naye. Mkuu wa shule akafikishiwa taarifa kuwa nina mahusiano ya kimapenzi na yule mtoto.
Moyo wangu na Mungu pekee ndio walikuwa mashahidi. Nilikosa cha kujibu.
Nilijaribu kujiweka mbali naye lakini moyo ulinambia kuwa kuna jambo natakiwa kulijua.
Nikaendelea kuwa karibu naye. Hatimaye mkuu wa shule akanisimamisha kufundisha pale kwa tabia yangu ya kufanya mapenzi na mwanafunzi.
Nilijitetea lakini sikueleweka. Nikamwachia Mungu……
Licha ya kusimamishwa kazi, niliendelea kufuatilia nyendo za yule binti aliyeitwa Janeth.
Kila alipotoka shule nilimvizia njiani na kumnunulia chakula, kisha tunazungumza kidogo.
Aliponiamini kama kaka yake ndipo nikajieleza dukuduku langu.
“Janeth…” nilimuita.
“Bee kaka ….” Aliitika huku akinitazama.
“Nyumbani unaishi na wazazi.”
“Ndio naishi na mama..baba huwa anasafiri safari.”
“Mama yako ana watoto wangapi?”
“Mama yangu alikufa….alikufa nikiwa mdogo hata simkumbuki” Alijibu kwa sauti ya chini.
“Kwa hiyo unaishi na mama mdogo.”
“Ndio.”
“Unampenda mama mdogo?”
Swali hili likaikatisha furaha ya Janeth. Akaanza kulia, alilia bila kukoma, Janeth alilia kwa uchungu hadi nikajisikia vibaya. Nilimbembeleza kisha sikumuuliza tena.
Siku zikaenda bila kumuuliza chochote..
Baada ya siku kumi, ilikuwa siku ya michezo pale shuleni, hivyo hapakuwa na masomo.
Janeth alichelewa kuja shule, nilimngoja uwanjani, hadi alipofika majira ya saa nne.
Nikamwambia twende kunywa chai.
Siku hiyo nilimpeleka mbali kidogo, tukanywa chai, kisha tukakaa mahali palipokuwa wazi.
Nikaleta tena mjadala mezani.
Ni kuhusu maisha ya Janeth.
Alikataa kabisa kusema lolote, nilimshawishi sana.
“Usiogope mimi ni kaka yako.” Nilimpooza.
Janeth badala ya kusimulia akaanza kulia tena.
“Ataniua mama nikisemaaaa” alilalamika.
Nikambembeleza hatimaye akanieleza jinsi anavyonyanyaswa na mama yake.
“Mama hanipendi hata kidogo, ananipiga na kuninyima chakula, hapendi nije shule, vyombo tunavyotumia usiku hataki nivioshe usiku na hataki niwahi kuamka asubuhi, nikiamka natakiwa kufanya kazi zote, kufagia uwanja, kudeki nyumba, kuosha vyombo kisha ndipo nije shule. Baba akiwepo anajidai kunijali sana…”
Alijieleza.
“Ni hayo tu Janeth….niambie kila kitu.”
“Akijua ananiua alisema….”
“Kwani amewahi kukutesa vipi..”
Ni hapa Janeth alivyozungumza huku analia kilio ambacho hakitatoka masikioni mwangu kamwe.
Siku moja, alichelewa kuamka, ilikuwa siku ya mapumziko.
Mama yake alipomwamsha, aliitika na kupitiwa usingizi tena.
Mama aliporejea mara ya pili, alikuwa na mti mkavu, alimpiga nao kichwani na popote pale katika mwili, alipoona hiyo haitoshi akamvua nguo, akausokomeza katika sehemu za siri, aliuigiza hovyohovyo, ukuni huo ulikuwa wa moto.
Yeyote mwenye moyo wa nyama ajifikirie ukuni wa moto ukazamishwa sehemu za siri za mtoto wa darasa la sita.
Nilitokwa machozi.
Nikawahi kujifuta hakuona.
“Baba yeye alisemaje….”
“Baba ni mkali na hapendi kunisikiliza na mama aliniambia nikiambia mtu ananiua mara moja.” Alijibu kwa huzuni.
“Nikija na dada yangu tunaweza kukuona ulivyounguzwa..”
“Ndio…” alinijibu.
Sikutaka kulaza damu nikampigia simu rafiki yangu wa kike.
Nikamuuliza kama yupo kwake, alikuwepo.
Nikaongozana na Janeth.
Tukafika, Janeth akatoa nguo zote.
Ilihitaji moyo wa kiuaji sana kutazama mwili wa Janeth mara mbilimbili.
Alitisha, hakika alikuwa ameunguzwa vibaya na vidonda vilikuwa havijapona vizuri.
Dada yule alishindwa kujizuia alimlazimisha Janeth twende kwa mama yake amkabiri na kumpa kipigo. Nikamzuia.
Hata mimi nilikuwa na hasira kali. Lakini sikutaka kuiruhusu ifanye kazi.
Nikachukua kamera, nikampiga picha Janeth katika yale makovu.
Mbio mbio nikaenda polisi, kituo cha haki za watoto nikaelezea mkasa ule huku nikishindwa kujizuia machozi.
Nikawaonyesha na picha.
Tukaongozana nao hadi nyumbani kwao Janeth.
Mama yule akakamatwa bila kutarajia.
Nilitamani kumrukia nimng’ate lakini haikuruhusiwa.
Sheria ikafuata mkondo. Janeth akaanza kupokea tiba.
Yule mama akahukumiwa kwenda jela miaka sita..hadi sasa yupo jela.
Mume wake alitozwa faini kubwa kwa kosa la kutofuatilia maendeleo ya mtoto wake kiafya……..
Mimi nilirudishwa kazini, kwa heshima kubwa. Heshima ya nkumkomboa mtoto.
***Akina JANETH wapo mtaani kwako…..usiwaangalie na kuwaacha tu…hebu jaribu KUWA SAUTI YAO….hawawezi kusema…hebu sema badala yao…….wanalia kisikie kilio