Enzi zetu ilikuwa raha sana, najua mtabisha maana
mnajiona wajanja, lakini aise mmekosa mengi
sana. Siku hizi shida tupu, nikikumbuka enzi zetu
nawaonea huruma.
ule kwetu enzi zile ukitaka kuoa, unapeleka posa
ikikubaliwa unapangiwa mahari, mara nyingi
mahari ilikuwa ng’ombe wawili, mbuzi na kondoo
mmoja, raha yake ilikuwa baba yako ndiye
anayekulipia mahari.
Bibi harusi alikuwa hana gharama kabisa, akijitahidi
kununua gauni lolote jeupe na kilemba cheupe,
kamaliza vazi la harusi na bwana harusi hapo
kuonesha unajali unajitahidi unamnunulia
mchumba raba nyeupe, mchezo unakwisha
hudaiwi kitu.
Siku ya harusi huna haja ya gari wala baiskeli, bibi
harusi anatembea kwa mguu toka kwao mpaka
kwako, mnaanza maisha, mambo simpo kabisa.
Ng’ombe walipoanza kuwa shida hasa kwa watu
wa mjini, ndiyo ikaanza taratibu ya kulipa fedha
badala ya wanyama kama mahari, ng’ombe
alikuwa shilingi mia tano, mbuzi na kondoo shilingi
thelathini.
Ukipangiwa mahari ya ng’ombe wawili na mbuzi
wawili unalipa shilingi alfu moja na sitini, tena kwa
kawaida mahari huwa haikamilishwi, hivyo
ikikushinda kidogo hakuna kesi.
Sasa zama hizi kiboko, mtu unapangiwa mahari
shilingi milioni mbili, halafu lazima utafute suti ya
laki tano, magari ya kifahari, mipombe,
ukumbi, mivideo, kitu kama milioni kumi lazima
zikutoke. Halafu kuna
hiki kichekesho kipya cha kuleta mizawadi kwenye
ukumbi, vitanda
makabati mafriji, mafriza.
Vurugu tupu. Wiki moja baada ya harusi
maharusi wako hoi kifedha wanaanza kukopa hata
hela ya kula. Acha
bwana enzi zetu ilikuwa raha sana.